Dar es Salaam. Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe (pichani) amezungumzia kukosekana kwa Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk Willibrod Slaa katika vikao vya chama hicho
vinavyoendelea jijini, akisema: “Nitazungumzia suala hilo muda muafaka
ukifika.”
Mbowe alisema hayo jana katika Hoteli ya Ledger Plaza Bahari Beach kilipokuwa kinafanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema jana.
“Siwezi
kusema zaidi ya hapo,” alisema Mbowe alipoulizwa sababu za kutokuwapo
Dk Slaa katika vikao hivyo muhimu na kuongeza atatoa baadaye, mrejesho
wa kikao hicho.
Kauli hiyo ya Mbowe haikuondoa wingu
zito lililotanda Chadema baada ya kutoonekana hadharani kwa kiongozi
huyo katika matukio manne muhimu ya chama hicho kikuu cha upinzani,
tangu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ajiunge nacho.
Tofauti
na Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika alionekana jana kwa
mara ya kwanza katika kikao hicho na kufuta uvumi uliokuwa umesambaa
kuwa alikuwa na mpango wa kuachana na Chadema kama inavyodaiwa kwa Dk
Slaa.
Viongozi hao walianza kutoonekana katika shughuli
za chama tangu Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 na kukabidhiwa
fomu ya kugombea urais Julai 30 na juzi Agosti Mosi alipozirejesha.
Hata
hivyo, viongozi waandamizi wa Chadema wamesema suala la kutokuwapo kwa
Dk Slaa halipaswi kukuzwa kwa kuwa ‘anafanya kazi nyingine za chama.’
Alipoulizwa
jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema: “Suala la
kutokuwapo Dk Slaa ni kitu cha kawaida, anafanya kazi nyingine huko,
lakini pia kuna wasaidizi wake hapa ambao ni sisi manaibu. Mlikuwa
mnazungumzia Mnyika naye haonekani, si huyo. Hatuwezi kuendelea kujibu
‘rumors’ (uzushi) wa kwenye mitandao… nyie subirini si tupo mtaona kama
yupo au la.”
Mnyika atinga kikaoni
Jana, Mnyika alionekana katika viwanja vya hoteli hiyo lakini alikataa kuzungumzia kwa undani suala hizo.
“Siwezi
kuzungumza chochote,” alisema Mnyika na hata alipoulizwa ni lini
atawaeleza Watanzania juu ya kutoonekana kwake alisisitiza mara tatu
kuwa “Siwezi kuzungumza chochote.”
Chama hicho
kinaendelea na mfululizo wa vikao vya vyombo vya juu ambapo leo
kinatarajia kutafanya kikao cha Baraza Kuu kabla ya Mkutano Mkuu kesho
kumpitisha mgombea wa urais kesho.

No comments:
Post a Comment